Japo kizazi cha sasa kinalaumiwa kwa kuwa na utovu wa nidhamu, wazazi wa sasa pia wanachangia. Ni wakati huu tu ambapo wavyele watashikana mashati, kuraruana marinda na kurushiana makonde eti kwa sababu mtoto amerekebishwa na mtu asiye mama yake au baba yake. Jambo hili huwafanya watoto hawa kufura vichwa. Wengi wao huishia kutoambilika, kukanyika wala kusemezeka abadan katan. Ni wawa hawa watoto ambao humezwa na shinikizo la rika na kuanza kuwa wastaarabu wa kuiga mienendo duni ya ushoga na uraibu wa dawa za kulevya, wizi na hata ngono za kiholelaholela. Japo baadhi ya wazazi wa watoto hawa hung’ang’ana kimaisha ili kuyakimu mahitaji yao ikiwemo elimu,
wao wanapoenda shuleni hubebwa na mawimbi ya hisia na kuanza kuogelea katika bahari ya mapenzi. Wengine huwageuka wazazi wao na kuwadhuru kwa cheche za maneno au hata kuwapiga! Huzuni ulioje! Matokeo huwa ni mimba au magonjwa ya Zinaa mengine yasiyo na tiba. Wazazi wa watoto watoro sampuli hii husongwa na mawazo, mishtuko ya moyo na hata wengine huaga dunia kabla ya siku zao kukatika duniani. Dawa mujarabu kwa kizazi cha sasa ni wazazi kuwa na msimamo thabiti pasi na kuwadekeza kama yai la bata bukini. Watenge muda ili wawaongeleshe wana wao. Wengi wa wazazi wa sasa wako ‘bisi’ kutwa kucha. Wamewachia walimu majukumu ya malezi nao wakiwa tu mbioni kusaka riziki huku wakiwacha wanao na kiziki cha ‘MAISHA NI YANGU’ Wajue kuwa, TEKE LA KUKU HALIMUUMIZI MWANAWE.” Na Mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe.
Ukweli mtupu. Wazazi wasiwadekeze Watoto. Lau sivyo kizazi kitazama!