FASIHI

MAANA YA FASIHI

Fasihi ni Sanaa ambayo hutumia lugha ya kiufundi kuwasilisha ujumbe au kusimulia visa.

Tanzu za fasihi ni mbili:

  1. Fasihi andishi-Ushairi, riwaya, hadithi fupi, tamthilia na novela

Ushairi andishi-hutumia lugha ya mkato na mnato ili kuwasilisha ujumbe kwa hadhira lengwa

Ushairi simulizi-huhifadhiwa akilini

  • Fasihi Simulizi-Mazungumzo{dayolojia baina ya watu wawili, huwa mafupi kuliko tamthilia na huwasilishwa kwa hadhira moja kwa moja}, hadithi, ngano{Kwa njia yam domo}, maigizo{Hutokea jukwaani}, nyimbo, semi,

BAADHI YA TOFAUTI KATI YA FASIHI SIMULIZI NA ANDISHI

  • Fasihi simulizi huhifadhiwa akilini ilhali andishi huhiadhiwa vitabuni
  • Fasihi simulizi huweza kupitishwa kutoka kizazi hadi kingine ila andishi husomwa na hadhira lengwa .
  • Fasihi simulizi huwa na hadhira hai nayo andishi inaweza kusomwa
  • Fasihi simulizi ni milki ya jamii ilhali andishi ni milki ya mtu binafsi.

FASIHI INA UMUHIMU GANI HASA?

Dhima ya fasihi katika jamii ni nyingi si haba

  1. Kuburudisha jamii-Watu hukusanyika ili kuburudika na kufurahishwa na uwasilishaji
  2. Kuelimisha-Kutokana na uwasilishaji wa fasihi, watu hupata mafunzo na kujirekebisha
  3. Hudumisha maadili mema katika jamii kwa kuonya na kunasihi jamii kufwata mwelekeo chanya.
  4. Kuunganisha jamii-Nyimbo, maviga na vichekesho huwaleta watu pamoja
  5. Kukuza lugha-Mbinu za lugha zinazotumika katika fasihi ni nyingi mno. Lugha inakuzwa pakubwa
  6. Husaidia kuhifadhi kumbukumbu za mila, tamaduni na itikadi za jamii mbalimbali
  7. Hukuza uwezo wa kufikiria-Wanaoshiriki katika kazi za fasihi huwa na akili pevu na ubunifu unaowasaidia kuikiri sana ilikupata suluhisho.

MAUDHUI NA DHAMIRA KATIKA FASIHI

Maudhui-Ni jumla ya masuala makuu yanayoangaziwa katika kazi ya fasihi. Ni ujumbe mkuu ambao mwandishi hunuia kupitisha kwa hadhira yake.

Dhamira-Ni lengo au kile ambacho mwandishi wa kazi ya fasihi anakusudia kimfikie msomaji.

LENGO LA DHAMIRA NI LIPI HASA?

  1. Kuhamasisha
  2. Kuonya
  3. Kuelekeza
  4. Kukashifu
  5. Kusifu

MAUDHUI HUCHAMBULIWA VIPI KATIKA KAZI YA FASIHI?

Maudhui katika fasihi huchambuliwa kwa kurejelea dondoo. Kwa mfano:

  • Ndoa za mapema- Mwanzoni wa aya ya kwanza, Binti Akiba anapanga njama ya kumwoza bintiye kwa lazima.
  • Elimu-Katika aya ya tatu sentensi ya mwisho, Bw. Somo anaishauri jamii kuwapeleka watoto shuleni
  • Funzo katika faishi huelezwa vipi?- Kitendo cha  paka kumpa chakula panya kinawacha funzo la  kuwa pevu na wenye fikra komavu.
  • Kitendo cha Anasa kupata gonjwa hatari la zinaa kinatuonya dhidi ya tabia za ukware na ukahaba.

NOVELA

Novela-Ni utungo wa fasihi andishi ulioandikwa katika lugha ya kinathari. Mrefu kuliko hadithi fupi lakini mreu kuliko riwaya.

Lugha ya nathari- Ni lugha yenye mtiririko mwepesi wa moja kwa moja.

NOVELA HUWA NA NINI HASA?

  • Ina wahusika wakuu na wahusika wadogo
  • Wahusika wadogo huwasaidia wahusika wakuu kuafikia lengo au dhamira ya mwandishi
  • Matendo na migogoro yote muhimu katika novela huwahusu wahusika wakuu.
  • Wahusika wakuu ni nguzo kwa sababu ni wao ndio wanaoiendeleza hadithi nzima
  • Huwa na ploti sahili-Mfwatano au mfululizo wa matukio{ Pia huitwa msuko}
  • Huwa na mandhari-Kumsaidia msomaji kuelewa yanayozungumziwa na kuweka matukio katika miktadha
  • Huwa na maudhui machache yanayokuzwa kwa uchache huku dhamira ya mwandishi ikijitokeza.

MANDHARI MBALIMBALI KATIKA NOVELA

Mandhari huonyesha mahali ambapo matukio ya hadithi hutokea au mazingira ambamo hadithi inasimuliwa.

MAZINGIRA HUONYESHA NINI HASA?

  1. Mahali halisi ambapo hadithi inatokea
  2. Jamii ambayo hadithi  inasimuliwa
  3. Utamaduni wa jamii husika

Mandhari pia huonyesha wakati ambapo matukio katika hadithi yanatokea. Hujumuisha:

  1. Siku ambayo tukio linatokea
  2. Kipindi ambacho hadithi inasimuliwa. Kwa mfano Baada ya ukombozi, likizo n.k

Swali linaweza kuja vipi? Tambueni aina hizi za mandhari katika novela uliyoisoma.

UCHAMBUZI WA WAHUSIKA KATIKA NOVELA

Wahusika huwa ni viumbe wanaopatikana katika kazi ya fasihi.

Wahusika katika Novela huchambuliwa kwa kuzingatia:

  1. Sifa za wahusika hao. Kwa mfano-Katili, fisadi,dikteta,kaidi, tapeli, karimu, Mwenye ubinafsi, mwenye bidii n.k
  2. Uhusiano wake na wahusika wengine. Athari ya matendo yake kwa wengine ni zipi? Wanajengana kivipi?
  3. Mchango wa mhusika katika kutatua tatizo. Kwa mafono, Amani anawashauri wengine kutokuwa wepesi wa hasira. Bw. Ukweli anasisitiza kuwa ufisadi huathiri uchumi wa taifa

KUMBUKA: Mbinu ya lugha ya kuvipa uhai vitu visivyokuwa na huai ni uhaishaji/uhuishaji/ tashhisi

Je, kuna wahusika aina ngapi katika kazi ya fasihi?

Mhusika fanani-Pia huitwa mtambaji au msimulizi. ‘Wajukuu wangu, mimi ona nimekula chumvi nyingi. Miaka imeganda. Sasa nilichobaki nacho ni kuwapa ushauri. Naomba mufungue sikio la ndani ili msije mkajuta baadaye. Dunia tambara mbovu! Na ni mti mkavu ambao kamwe huwezi ukauegemea! Msiendelee na maadili yaliyooza. Mwishowe…

Fanani katika hadithi hii ni nani?_________________________

Hadhira ni gani katika hadithi hii?________________________

Hadhira-Hawa ni watu ambao wanasimuliwa hadithi

Je, Kuna aina ngapi za hadhira?

  1. Hadhira tendi– Ni hadhira inayoshiriki kikamilifu aidha kwa kuitikia au kupiga makofi.
  2. Hadhira tuli-Ni hadhira inayotulia na kumsikiliza mtambaji bila kuchangia

PLOTI

Ploti ni matukio yanayoijenga hadithi. Huonyesha jinsi matukio yanavyofwatana

Ploti huanza kwa tukio kuu au tatizo linalomkumba mhusika. Tatizo pia huitwa mgogoro

Ploti huishia kwa suluhisho la mgogoro huo

SEHEMU TATU KUU ZA PLOTI NI ZIPI HASA?

  1. Mwanzo-Hapa ndipo tatizo linalokumba mhusika au wahusika hujitokeza
  2. Kati-Mhusika au wahusika wanatia juhudi za kukabiliana na tatizo au mgogoro
  3. Mwisho-Huonyesha jinsi tattizo lilivyotatuliwa. Kwa mfano, mhusika anashinda! Msomaji kuachwa katika taharuki…au mhusika kushindwa kabisa kupata suluhu.

Je, Ploti huchambuliwa vipi katika Novela?

Baada ya kusoma Novela, Chambua ploti katika vipengele vifwatavyo:

  1. Mwanzo-Orodhesha matukio muhimu kisha tatizo kuu
  2. Kati-Orodhesha matukio muhimu kisha tatizo kuu
  3. Mwisho-Orodhesha matukio muhimu kisha onyesha suluhu la tatizo

Tumia wakati uliopo hali timilifu. Kwa mfano: Maimuna anaamua kuondoka na kuelekea mtoni usiku wa manane…

Swali linaweza kuulizwa vipi?

Bainisheni sehemu hizi katika ploti ya kifungu ulichokisoma.

  1. Mwanzo       b.Kati           c. Mwisho

NYIMBO

Nyimbo ni mfano wa fasihi simulizi

Aina za nyimbo ni pamoja na:

  1. Nyimbo za watoto au chekechea
  2. Nyimbo bembelezi
  3. Nyimbo za kazi
  4. Nyimbo za dini

Nyimbo za watoto au chekechea ni nyimbo zanazoimbwa na watoto wanapocheza. Pia, huimbwa shuleni ili kuwashirikisha katika masomo.

SIFA ZA NYIMBO ZA WATOTO NI ZIPI HASA?

  1. Huwa fupi
  2. Huwa na maneno mepesi
  3. Huwa na uradidi wa maneno
  4. Huwa na maneno ya kujibunia
  5. Huwa na sehemu ya kiongozi na sehemu ya hadhira
  6. Huimbwa na watoto
  7. Huambatana na ishara zinapoimbwa

Nyimbo za bembelezi ni nyimbo zinazoimbiwa watoto ili waweze kutulia au hata kulala.

Pia huitwa bembea au pembejezi.

SIFA ZA NYIMBO ZA BEMBELEZI NI ZIPI HASA?

  1. Huimbwa na mzazi au mlezi kwa lengo la kumbembeleza mtoto
  2. Huimbwa kwa utaratibu na kwa sauti ya chini ili kuongoa mtoto
  3. Huwa fupi
  4. Huwa na urudiaji wa maneno
  5. Lugha inayotumika ni ya ushawishi na ahadi tele kwa mtoto.

NYIMBO ZA KAZI

Nyimbo za kazi huimbwa mtu anapofanya kazi

Kwa mafno: Uvuvi, ukulima, usgaji nafaka n.k

Nyimbo hizo huwa na ujumbe maalum kama vile: Umuhimu wa kazi, ushirikiano au hata maadili.

VIONGOZI KATIKA NYIMBO

  1. Kiongozi wa wimbo
  2. Waimbaji
  3. Hadhira
  4. Wapigaji ala za Muziki
  5. Wahusika wanaoimbwa au kutajwa katika wimbo huo

WAHUSIKA HUCHAMBULIWA VIPI?

  1. Kutaja ni kina nani katika wimbo
  2. Ni wa aina gani? Wakuu au wadogo
  3. Sifa zao
  4. Mchango wao katika uwasilishaji wa wimbo
  5. Uhusiano wao na wahusika wengine katika wimbo

Swali linaweza likaulizwa vipi?

  1. Tambua wahusika katika wimbo huo
  2. Chambua wahusika katika wimbo huo ukirejelea:
  3. Sifa zao
  4. Umuhimu wao
  5. Eleza mafunzo kutokana na wahusika katika wimbo huo

MBINU ZA LUGHA KATIKA FASIHI

Mbinu hizi pia huitwa mbinu za kimtindo au tamathali za lugha.

  1. Takriri au uradidi-Huu ni urudiaji wa maneno kwa lengo la kusisitiza ujumbe. Ahsante! Ahsante sana!
  2. Tasfida-Ni hali ya kutumia maneno ya adabu na heshima
  3. Majazi-Ni hali ya kuvipa viumbe majina kwa mujibu wa sifa zao
  4. Tashbihi-Ni ulinganisho wa kitu na kingine. Mjanja kama sungura
  5. Sitiari-Ni ulinganisho usio wa moja kwa moja. Hautumii maneno ya kulinganisha. Yeye ni sungura
  6. Tanakali za sauti/Viigizi-Ni uigaji wa sauti ambazo huashiria kufanyika kwa kitendo fulani.
  7. Nahau/ semi-Fungu la maneno yenye maana tofauti-Kula mwata[pata taabu]
  8. Methali-Ni fungu lenye maana fiche. Huelezea kuhusu ukweli Fulani wa maisha.
  9. Chuku-Ni maneno yasiyo ya kweli. Mfano, aibu ilimtuma mawinguni na kujifungia huko hadi wa leo.
  10. Tashhisi/uishi-Ni hali ya kuvipa vitu visivyo na uhai sifa za uhai. Mfano: Kengele ilipolia sote tuliondoka kwa haraka.
  11. Kinaya-Ni tukio ambalo huwa kinyume na matarajio. Mfano, Mfalme aliomba watoto msaada wa chakula ili asife kwa njaa.
  12. Balagha-Maswali yasiyohitaji majibu ambayo hujitokeza katika hadithi
  13. Taswira-Ni maneno yanayotumia jozi jozi ili kuleta picha Fulani ya tukio. Pua na mdomo_ Inakupa picha ya ukaribu! Ardhi na mbingu-Inakupa picha ya utengano

MIGHANI-Ni hadithi za kihistoria ambazo husimuliwa kuhusu mashujaa au majagina wa jamii Fulani. Pia huitwa visakale.{ Huzungumzia visa vilivyotokea hapo kale}. Mfano, Lwanda magere wa Luo, Koome Njue wa Meru, Sakagwa wa Kisii, Wangu wa Makeri-Kikuyu  na Elija wa Nameme Bukusu.

Mighani hutumia mbinu za lugha.

SIFA ZA MIGHANI NI ZIPI HASA?

  1. Huhusu mashujaa wa jamii Fulani
  2. Wahusika hupewa sia za kiajabu
  3. Mashujaa huwa na uwezo uliozidi wa binadamu
  4. Mhusika huikomboa jamii yake dhidi ya maadui
  5. Wahusika hupambana na hali ngumu
  6. Mhusika hufa kifo cha huzuni hasa baada ya usaliti kutoka kwa mtu wake wa karibu

NI NINI HUZINGATIWA KATIKA UWASILISHAJI WA MIGHANI?

  1. Lugha inayoeleweka na hadhira
  2. Usimulizi huambatana na maigizo, maonyesho na vifaa halisi
  3. Mtambaji huhusisha hadhira kwa kuwauliza maswali
  4. Mwasilishaji anaweza kutumia ishara ili kusisitizia anachokisimulia

TAMTHILIA

Ni utanzu wa fasihi andishi ambao huwasilishwa kupitia mtindo wa kimazungumzo  kati ya wahusika.

Tamthilia ni mchezo wenye maudhui na dhamira  inayolenga kuigizwa jukwaani.

Katika tamthilia huwa na maelekezo

SIFA ZA TAMTHILIA NI ZIPI HASA?

  1. Hugawanywa katika sehemu zinazoitwa maonyesho
  2. Kila onyesho huendeleza hoja kuu
  3. Huandikwa kwa mtindo wa kimazungumzo
  4. Huwa na maelekezo ya jukwaani ambayo hufafanua tabia na hisia za wahusika
  5. Huandikwa kwa lengo la kuigizwa mbele ya hadhira
  6. Huwa na utangulizi, mgogoro, kilele na hitimisho inayoashiria kutatuliwa kwa mgogoro.
  7. Uteuzi wa mapambo jukwaani hutegemea dhamira na maudhui ya tamthilia ili kufanikisha uigizaji.

JE, MSOMAJI HUWEZA KUJUA VIPI  SIFA ZA WAHUSIKA KATIKA TAMTHILIA?

  1. Kupitia matendo ya wahusika hao
  2. Yanayosemwa na wahusika wengine kuwahusu
  3. Kauli wazazotumia wahusika hao
  4. Yanayosemwa na mwandishi kuwahusu kupitia jukwaani.

VISASILI NI NINI?

Ni hadithi za kihistoria ambazo huelezea asili/chanzo au chimbuko la mambo mbalimbali katika jamii.

Mbona Visasili hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine? –Kwa sababu hujikita katika Imani ya jamii husika.

Pia huelezea asili ya maumbile mbalimbali kama vile milima au mito.

Wahusika katika visasili ni kina nani hasa?-Binadamu, wanyama, mimea, mawe au miungu.

SIFA ZA VISASILI NI ZIPI HASA?

  1. Huelezea chimbuko au asili ya jamii Fulani.
  2. Husimulia mambo ya kale
  3. Wanajamii husika huamini visasili kuwa vya kweli
  4. Hpitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine
  5. Hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
  6. Huwa na wahusika mbalimbali
  7. Huhusisha masimulizi ya kiimani na dini

NI NINI HUZINGATIWA KATIKA UWASILISHAJI WA MIGHANI?

  1. UJUMBE-Hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali
  2. WAHUSIKA-Viumbe au vitu vinavyotumika kupitisha ujumbe
  3. PLOTI-Ni namna matukio katika kisasili yanavyofwatana kutoka mwanzoni hadi mwisho
  4. MGOGORO-Huwa ni mitazamo mbalimbali katika kisasili ambayo ambayo mara nyingi huleta matatizo.

HURAFA NA HEKAYA

Hurafa-Ni hadithi ambazo  wahusika wake ni wanyama ila hupewa sifa za binadamu kama vile kuzungumza n ahata kuongoza.

Hekaya-Ni hadithi ambazo zina mhusika mjanja anayetumia ujanja wake kujifaidi. Pia huitwa hadithi za kiayari

KUNA TOFAUTI GANI KATI YA HURAFA NA HEKAYA?

Wahusika wote katika hurafa huwa wanyama ila si lazima wahusika wawe wanyama katika hekaya.

Hurafa hazina mhusika mjanja kama ilivyo kwenye hekaya

NINI NINI HUZINGATIWA KATIKA UWASILISHAJI WA HADITHI

  1. Kiini cha hadithi-Huu ni ujumbe au tukio lenyewe katika hadithi. Huonyeshwa kupitia mgogoro
  2. Kiwango cha lugha-Uteuzi wa lugha anayotumia msimulizi hutegemea umri wa hadhira yake
  3. Mpangilio wa matukio-Matukio hufwatana kwa njia ya moja kwa moja ili hadithi ieleweke kwa urahisi.
  4. Sauti-Msimulizi anastahili kutumia sauti inayosikia vizuri huku akizingatia kiimbo. {kupandisha na kuzusha sauti kwa kutegemea hisia}.
  5. Ishara za mwili-Matumizi ya ishara za mwili kama vile uso na mikono huvutia hadhira
  6. Mbinu au fomulae ya kutanguliza na kumaliza-Hadithi huanza na kuisha kwa fomula maalum. Kwa mfano: Hadithi! Hadithi! Paukwa! Pakawa. Ya kumazia ni kama vile: Hadithi yangu ikaishia hapo…au Wakaishi raha mustarehe.
Summary
UCHAMBUZI WA FASIHI GREDI 7/8
Article Name
UCHAMBUZI WA FASIHI GREDI 7/8
Description
Uchambuzi huu utawafaa wanafunzi
Author
Publisher Name
Ibuka FM
Publisher Logo

Leave a Reply